Mkutano wa ngazi ya juu wa kikanda kuhusu homa ya Nyani (Mpox) barani Afrika umeanza jana mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mkutano huo wa siku tatu unawakutanisha pamoja mawaziri wa Afya kutoka barani Afrika, kwa lengo la kutunga mikakati ya pamoja ili kukinga na kudhibiti kwa ufanisi ugonjwa huo katika bara hilo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC) Jean Kaseya amesema, ni lazima kuizuia DRC kuwa chanzo cha maambukizi ya kuvuka mpaka, na ushirikiano wa nchi hizo za Afrika unapaswa kutoa kipaumbele kwa afya za watu walioathirika na ugonjwa huo.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani nchini DRC, Boureima Hama Sambo amesema, Zaidi ya kesi 4,500 za ugonjwa huo zimeripotiwa nchini DRC tangu mwanzo wa mwaka huu, na watu 300 wamefariki kutokana na homa hiyo.