Mamlaka ya Usimamizi wa Mipaka ya Afrika Kusini (BMA) imesema jumla ya wasafiri milioni 1.12 walipita kwenye forodha 71 za kuingia nchini humo wakati wa mapumziko ya Pasaka ya mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 24 ikilinganishwa na mapumziko hayo mwaka jana.
Kamishna wa mamlaka hiyo Bw. Michael Masiapato alisema kwenye mkutano na wanahabari kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo mjini Johannesburg, forodha ya Lebombo kwenye mpaka na Msumbiji, na forodha ya Beitbridge kwenye mpaka na Zimbabwe ni forodha tatu zilizopokea wasafiri wengi.
Hata hivyo Bw. Masiapoato amesema jumla ya watu 3,841 waliokuwa wakijaribu kuingia Afrika Kusini kinyume cha sheria wakati wa Pasaka walikamatwa, wengi wao ni wale waliokamatwa bila hati katika sehemu zilizo hatarini za mpaka.