Baraza la usalama laitisha mkutano wa dharura kuhusu shambulizi la Iran dhidi ya Israel
2024-04-15 09:43:11| CRI

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha mkutano wa dharura kuhusu shambulizi la Iran dhidi ya Israel, ambapo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Guterres amezitaka pande zote zijizuie kwa kiasi kikubwa.

Bw. Guterres amesema eneo la Mashariki ya Kati linakumbwa na tishio la mgogoro wa pande zote, kwa sasa kuna haja ya kutuliza tishio hilo na kujizuia kwa kiasi kikubwa. Katiba ya Umoja wa Mataifa inapiga marufuku vitendo vya kukiuka kwa nguvu ukamilifu wa ardhi au uhuru wa kisiasa wa nchi zote, na ni lazima msingi wa kutoshambulia ubalozi na wanadipolomasia uheshimiwe.

Bw. Guterres amesema jumuiya ya kimataifa ina jukumu la pamoja la kuwasiliana na pande husika, na kuzuia kupamba moto kwa hali ya sasa, na kutafuta kutimiza usitishwaji vita kwenye ukanda wa Gaza, na kufanya juhudi kuhimiza kuachiwa huru kwa mateka, na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafika wenye mahitaji bila vizuizi. Pia jumuiya ya kimataifa ina jukumu la pamoja kusimamisha vitendo vya kimabavu kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Jordan, kutuliza hali ya wasiwasi kwenye mpaka kati ya Israel na Lebanon, na kurejesha usalama wa usafiri kwenye bahari ya Sham.