Zanzibar kuwa mwenyeji wa mkutano wa anga wa EAC
2024-04-15 11:07:05| cri

Zanzibar inatazamiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa sita wa Mamlaka ya Uangalizi wa Usalama wa Usafiri wa Anga (CASSOA), unaotarajiwa kufanyika tarehe 16-17 Mei, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari, alitangaza kuwa mkutano huo utawakutanisha wadau wakuu wa sekta ya anga wakiwemo wa mashirika ya ndege, viwanja vya ndege, mameneja na maofisa usalama kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Bw Johari alibainisha kuwa mbali na mkutano huo kuangazia masuala endelevu ya mazingira katika sekta ya anga pia utajikita katika kuchunguza na kufufua sekta ya anga, kwa kuzingatia kurejesha imani ya watumiaji na kuongeza ufahamu wa fursa zinazohusiana na uvumbuzi wa sasa wa anga.