Thamani ya sarafu mpya ya Zimbabwe yaongezeka huku kukiwa na mashaka ya soko
2024-04-15 08:40:10| CRI

Thamani ya sarafu mpya ya Zimbabwe inayoungwa mkono na dhahabu, inayojulikana kama Dhahabu ya Zimbabwe (ZiG), imeongezeka kwa asilimia 1.1 dhidi ya dola ya Marekani katika wiki yake ya kwanza ya biashara.

Ongezeko hilo linaendana na ongezeko kubwa la bei ya dhahabu, linalochochewa na mahitaji ya wawekezaji kwenye mali salama.

Sarafu ya ZiG imechukua nafasi ya dola ya Zimbabwe ya zamani iliyoathiriwa na mfumuko wa bei na kuanza kufanya biashara Jumatatu, baada ya kuzinduliwa na Gavana wa Benki Kuu ya Zimbabwe John Mushayavanhu Aprili 5.

Licha ya mkanganyiko wa awali wa soko kuhusu sarafu hiyo mpya, benki nyingi na wafanyabiashara walifanikiwa kubadilisha dola ya Zimbabwe na kuwa ZiG. Hatua hii imeweka mazingira ya ZiG kutumika sambamba na sarafu nyingine za kigeni hadi mwaka 2030.