Mapacha wakongwe zaidi duniani walioungana, wamefariki wakiwa na umri wa miaka 62
2024-04-15 23:03:47| cri

George na Lori Schappell, ambao walikuwa mapacha wenye umri mkubwa zaidi duniani walioungana, walifariki Aprili 7 katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Pennsylvania huko Philadelphia.

Mapacha hao walizaliwa Septemba 18, 1961, huko West Reading, Pa., na kwa mujibu wa Rikodi za Guinness hadi wanafariki walikuwa na umri wa miaka 62 na siku 202. Walikuwa wakubwa kwa miaka tisa kuliko mapacha wanawake wanaochukua nafasi ya pili ambao wamezaliwa wakiwa wameungana kuwahi kurekodiwa.

Lori na George waliungana kichwani na walikuwa na miili tofauti. Guinness waliripoti kuwa walikuwa wameungana mafuvu ya kichwa na kutumia pamoja mishipa ya damu na 30% ya ubongo wao. Wakati Lori aliweza kutembea, George alikuwa anatumia kiti cha magurudumu ambacho kilikuwa kinasukumwa na Lori.