Flamingo mashuhuri wa Afrika watishiwa kutokana na kupanda kwa viwango vya maziwa
2024-04-16 22:54:47| cri

Watafiti walisema wikiende kwamba, maziwa ambayo flamingo hukusanyika kwa wingi barani Afrika yanazalisha chakula kidogo kwa ndege hao wa kuvutia wakati kiwango chao cha maji kinapoongezeka, na kutishia maisha ya spishi hiyo inayopendwa sana.

Robo tatu ya flamingo wadogo duniani wanaishi Afrika Mashariki na zaidi ya ndege milioni moja wanaweza kukusanyika kwa wakati mmoja kwenye maziwa kwa ajili ya malisho na kupandana.

Lakini maziwa hayo yanapopanuka na kufikia kiwango cha juu zaidi, wanasayansi wamegundua kwamba yanatoa mwani mchache sana ambao wanautegemea flamingo, na hivyo kuhatarisha spishi ambazo tayari zimepungua.

Mwandishi mkuu wa utafiti huu Aidan Byrne alisema hali hii inawafanya ndege hawa wa rangi ya waridi na wa kipekee wakimbie mbali na makazi yao ya kawaida hadi katika maeneo yasiyolindwa wakitafuta chakula.