Mjumbe wa Umoja wa Mataifa aonesha wasiwasi kuhusu unyanyasaji wa watoto nchini Zambia
2024-04-16 08:28:36| CRI

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mambo ya ukatili dhidi ya Watoto Bibi Najat Maalla, ameeleza wasiwasi wake kwamba ukatili dhidi ya watoto bado ni jambo la kila siku kwa watoto wengi nchini Zambia, licha ya nchi hiyo kuwa na sheria na sera za kuwalinda watoto.

Akiongea wakati akikamilisha ziara yake nchini Zambia, Bibi Najat amesema ukatili dhidi ya watoto unaendelea kuwa kero kubwa na hali halisi ya kila siku kwa watoto wengi.

Utafiti kuhusu ukatili dhidi ya watoto nchini Zambia umeonesha kuwa asilimia 41 ya wasichana na asilimia 49 ya wavulana waliripoti kufanyiwa au kushuhudia ukatili wa kimwili katika ngazi ya kaya, na asilimia 65 walionyesha kuwa walidhulumiwa shuleni. Bibi Najat amesema ongezeko la mgao wa bajeti kwa ajili ya huduma za msingi za ulinzi wa watoto lilikuwa muhimu katika kushughulikia tatizo la idadi ndogo ya wafanyakazi wa kijamii nchini Zambia.