Waziri wa mambo ya nje ya China azungumza na mwenzake wa Iran kwa njia ya simu
2024-04-16 08:59:51| CRI

Waziri wa mambo ya nje ya China Bw. Wang Yi jana Jumatatu alizungumza na mwenzake wa Iran Bw. Hossein Amirabdollahian kwa njia ya simu.

Bw. Amirabdollahian ameeleza msimamo wa Iran juu ya shambulizi dhidi ya ubalozi wake nchini Syria, akisema Iran ina haki ya kujilinda na kujibu ukiukaji wa mamlaka yake. Inapenda kujizuia na haina nia ya kuzorotesha hali ya kikanda. Pia amesema Iran inaunga mkono juhudi za China kuhimiza usitishwaji vita katika Ukanda wa Gaza, kurejesha utulivu na kuhimiza ushirikiano kati ya nchi za kanda hii.

Bw. Wang Yi amesema China inalaani shambulizi dhidi ya ubalozi wa Iran ambayo ni kinyume cha sheria ya kimataifa, na inapongeza msimamo wa Iran wa kutolenga nchi za kikanda na nchi jirani wakati inapolinda mamlaka yake. Inaamini Iran inaweza kudhibiti hali ya sasa na kutozidisha mgogoro. Ameongeza kuwa China inapenda kuendelea kuwasiliana na Iran katika kuhimiza suala la Palestina kutatuliwa kikamilifu, kwa njia ya haki na ya kudumu, na pia kuendelea kuimarisha ushirikiano halisi na Iran katika nyanja mbalimbali.