Tanzania, Rwanda na Zimbabwe zaungana na wenzao wa Afrika kusitisha matumizi ya dawa ya kikohozi ya watoto ya Benylin
2024-04-17 14:14:09| cri

Mamlaka za kudhibiti viwango vya dawa nchini Tanzania, Rwanda na Zimbabwe zimesitisha matumizi ya dawa ya kikohozi ya watoto iitwayo Benylin ya kampuni ya Johnson & Johnson kama hatua ya tahadhari baada ya Nigeria kusema vipimo vya maabara viligundua viwango vya juu vya sumu.

Nchi hizo zinaungana na Nigeria, Kenya na Afrika Kusini kusitisha matumizi ya dawa hiyo, ambayo hutumiwa kutibu kikohozi, homa na madhara mengine ya mzio kwa watoto. Afrika Kusini pia imesitisha matumizi ya dawa hiyo.

Uchunguzi wa kimaabara wa dawa hiyo uliofanywa na Nigeria ulionesha kiwango kikubwa cha kemikali ya diethylene glycol, ambayo imehusishwa na vifo vya watoto nchini Gambia, Uzbekistan na Cameroon tangu mwaka 2022 katika moja ya mawimbi mabaya zaidi ya sumu duniani inayotokana na dawa za kumeza.

Kemikali ya Diethylene glycol ni sumu kwa binadamu inapotumiwa na inaweza kusababisha figo kushindwa kufanya kazi.