Vyumba vya kuhifadhia maiti vya umma vyaelemewa huku mgomo wa madaktari ukiendelea
2024-04-17 23:12:55| cri

Athari za madaktari kutofika wodini na kutokwenda kwenye vyumba vya kufanyia upasuaji kutokana na mgomo unaoendelea wa madaktari nchini Kenya zinazidisha shinikizo kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti vya umma ambavyo kwa sasa vinaonekana kuelemewa zaidi.

Kwa mujibu wa Nation, shughuli zimeongezeka kupita kiasi katika vyumba tofauti vya kuhifadhi maiti kote nchini Kenya ambapo hali hiyo inatazamiwa kuwa mbaya zaidi baada ya mwezi mmoja.

Wakati serikali imeweka mkazo wake katika kushughulika na madaktari na maafisa wa kliniki ambao wameamua kuandamana barabarani kudai kuboreshwa kwa maslahi yao, maelfu ya wagonjwa wasio na msaada wameendelea kukwama na kudhoofika wakiwa majumbani mwao.

Licha ya Waziri wa Mambo ya Ndani Prof Kithure Kindiki kuapa kwamba atawalinda madaktari ambao wameamua kukaidi maagizo ya kurudi kazini, lakini bado mzigo wa wagonjwa wanaotafuta huduma muhimu katika hospitali za umma haujapungua.

Wakati misimamo mikali kati ya serikali na wafanyakazi wanaogoma ikiendelea, wagonjwa ambao hawana uwezo wa kutafuta huduma katika hospitali binafsi wanaendelea kupoteza maisha yao.