Kamati ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA) imetoa wito kwa nchi za Afrika kutumia fursa zinazotolewa katika maendeleo ya hivi karibuni katika sekta ya kimataifa ya betri na magari ya umeme (EV).
UNECA imetoa wito huo kwenye mkutano wa mapitio ya kitaalamu kuhusu utekelezaji wa ukanda maalum wa kiuchumi wa kuvuka mpaka kwa ajili ya sekta ya betri na magari ya umeme, utakaoanzishwa kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia kwa msaada wa UNECA na Benki ya Exim ya Afrika.
Mkurugenzi wa Ofisi Ndogo ya UNECA ya Kusini mwa Afrika Bibi Eunice Kamwendo, amesisitiza faida za mpango wa maendeleo ya betri na magari ya umeme katika nchi hizo mbili kwa mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi na mabadiliko ya kimuundo.
Mkurugenzi huyo pia amesema mpango huo unatoa fursa kubwa ya kubadilisha uchumi wa kanda na bara zima kupitia maendeleo ya madini.