Kenya imeandikisha raia wapatao milioni 20 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwenye ngazi ya shina kupitia matumizi ya teknolojia ya dijitali.
Katibu mkuu katika Wizara ya Afya Bi. Mary Muriuki amesema raia wameandikishwa na Wahamasishaji wa Afya Jamii (CHPs) walioajiriwa na Serikali mwezi Oktoba mwaka jana.
Kwa mujibu wa ofisa huyu lengo lao ni kuandikisha kaya zote nchini Kenya, mpaka sasa wameandikisha kaya milioni 4, kila moja ikiwa na wastani wa watu watano.
Bi. Muriuki amesema uandikishaji huo utarahisisha utoaji wa huduma za afya kupitia teknolojia ya dijitali, kama vile simu za mkononi, kwa kuwa Serikali sasa ina data za raia kuhusu changamoto za afya zinazowakabili.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Kenya inaendelea kupiga hatua kubwa kuelekea lengo la upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, licha ya mabadiliko yanayotokea katika idadi ya watu na magonjwa ya kuambukiza.