Mikakati ya Kuzuia Vifo Vya Mama na Watoto
2024-04-19 08:15:03| CRI

Afya ni muhimu katika ustawi wa watu, uimarishaji wa nguvu kazi na ukuzaji wa maendeleo ya taifa. Serikali mbalimbali duniani zimekuwa zikichukua hatua za kuboresha utoaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vipya vya afya, ukarabati wa vituo vilivyopo, utoaji wa vifaa tiba na upatikanaji wa dawa muhimu.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Umoja wa Mataifa (UN)iliyotolewa mwaka jana, maendeleo ya kimataifa katika kupunguza vifo vya wanawake wajawazito, akina mama na watoto yamepungua kwa miaka minane kutokana na kupungua kwa uwekezaji katika afya ya uzazi na watoto wachanga. Ripoti hiyo ilionesha kuwa zaidi ya wanawake na watoto milioni 4.5 hufariki kila mwaka wakati wa ujauzito, kujifungua au wiki za kwanza baada ya kuzaliwa, sawa na kifo 1 kinachotokea kila baada ya sekunde 7, hasa kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika au zinazoweza kutibika ikiwa huduma nzuri ingepatikana.

Ripoti hiyo, iliyopewa jina la “Kuboresha maisha na afya ya mama na watoto wachanga na kupunguza watoto wanaozaliwa wakiwa wamekufa, inatathmini data kuhusu vifo hivi ambavyo vina hatari na visababishi sawa, na kufuatilia utoaji wa huduma muhimu za afya. Kwa ujumla, ripoti imeonesha kuwa maendeleo katika kuboresha maisha yamedorora tangu mwaka 2015, kukiwa na karibu vifo vya uzazi 290,000 kila mwaka, watoto milioni 1.9 wanaozaliwa wakiwa wamekufa, watoto wanaokufa baada ya wiki 28 za ujauzito, na vifo vya watoto wachanga milioni 2.3, ambavyo ni vifo katika mwezi wa kwanza wa kuzaliwa. Hivyo kwa kuzingatia uzito na ukubwa wa tatizo hili, leo katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia mikakati ya kuzuia vifo vya mama na watoto.