Mwanamke aupeleka mwili wa marehemu hadi Benki akidaiwa Kujaribu Kumfanya Asaini Mkopo kwa Jina Lake
2024-04-18 10:34:57| cri

Katika tukio la kushangaza na la kustaajabisha katika tawi la benki la Bangu, Rio de Janeiro, Brazil, mwanamke alinaswa kwenye kamera akijaribu kumfanya mwanamume aliyekufa asaini mkopo kwa jina lake. Mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Erika de Souza Vieira Nunes, aliupeleka benki mwili wa marehemu Paulo Roberto Braga mwenye umri wa miaka 68.

Video ya mtandaoni ilimnasa Nunes akiwa benki na kujifanya kuwa mjomba yu hai na yuko tayari kutia sahihi hati hizo. Wafanyakazi wa benki walitilia shaka walipoona rangi ya mwanamume huyo iliyopauka na kurekodi tukio hilo huku Nunes akiinua kichwa cha marehemu na kujaribu kumshikisha kalamu.

"Mjomba unasikiliza, lazima usaini. Siwezi kukusainisha," alisikika akimwambia.

Licha ya ukimya wa marehemu, Nunes aliendelea kumtaka asaini hati hizo. Wahudumu wa afya walioitwa kwenye eneo la tukio walithibitisha kwamba Bw Braga alikuwa ameaga dunia saa chache zilizopita. Nunes, ambaye alidai kuwa yeye ni mpwa na mlezi wa Bw Braga, alikamatwa katika eneo la tukio huku polisi wakianzisha uchunguzi kubaini kama alitenda peke yake au alikuwa na wanafamilia wengine waliohusika. Mkopo ambao mwanamke huyo alitaka kuupata kwa njia ya ulaghai uliripotiwa kuwa ni takriban £2,500.