Wamarekani wenye asili ya Kiafrika bado wanakabiliwa na ubaguzi wa rangi
2024-04-18 14:39:23| Cri

Umoja wa Mataifa wiki iliyopita umeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi, na kaulimbiu ya mwaka huu ni “Muongo wa Utekelezaji wa Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Asili ya Kiafrika”. Wakati jamii ya kimataifa inajitahidi kuondoa ubaguzi wa rangi, Marekani, ambayo inajiita “mnara wa usawa, uhuru na haki” bado inakabiliwa na hali mbaya ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.

Miaka kumi iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza mwaka 2015 hadi 2024 kuwa Muongo wa utekelezaji wa Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Asili ya Kiafrika, likisisitiza kuimarishwa kwa hatua na ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuhakikisha watu wenye asili ya Kiafrika wana haki kamili za kiuchumi, kijamii, na kiutamaduni, na kushiriki katika nyanja zote za jamii kwa usawa.

Changamoto ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani hufuatiliwa sana na jamii ya kimataifa. Ingawa Marekani inadai kuwa ni nchi yenye usawa kwa watu wenye rangi tofauti, lakini ukweli unawaambia watu kwamba ubaguzi wa rangi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika bado uko katika kila kona ya jamii ya nchi hiyo.

Kwanza, kuna ubaguzi wa rangi wa wazi kati ya Wamarekani weusi na weupe katika nyanja ya kiuchumi. Idadi ya watu wenye asili ya Kiafrika ni zaidi ya asilimia 13 ya jumla ya watu nchini Marekani. Hata hivyo, hali yao ya kiuchumi iko mbali na kiwango hicho. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na vyombo vya habari vya Marekani, utajiri wa familia ya Wamarekani weupe ni wastani wa mara 6.5 wa familia ya Wamarekani weusi. Ubaguzi wa rangi pia upo katika soko la ajira, ambapo Wamarekani wenye asili ya Afrika wanakabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira, na wanafanya zaidi kazi ngumu na zenye mshahara mdogo.

Pili, kuna ubaguzi wa rangi katika mfumo wa utekelezaji wa sheria nchini Marekani. Uchunguzi umegundua kuwa Wamarekani wenye asili ya Kiafrika huwa wanahukumiwa vikali zaidi kuliko watu weupe wanapokabiliwa na mashtaka. Zaidi ya hayo, ubaguzi wa rangi uliofanywa na polisi dhidi ya watu weusi nchini humo umefichuliwa mara kwa mara. Mwaka 2020, kesi ya mwanamume mwenye asili ya Kiafrika George Perry Floyd kuuawa na afisa mweupe wa polisi ilisababisha maandamano kote nchini Marekani. Takwimu zilizotolewa na tovuti ya Marekani “Police Violence Map” zinaonyesha kuwa, katika mauaji ya polisi kuanzia mwaka 2013 hadi 2022, uwezekano wa watu weusi kuuawa na polisi ni mara 2.78 kuliko watu weupe, na huko Boston, Minneapolis na Chicago, kiwango hicho ni mara 20.

Tatu, ubaguzi wa rangi pia upo katika uwanja wa elimu. Kutoka elimu ya awali hadi elimu ya juu, wanafunzi wenye asili ya Kiafrika mara kwa mara wanatendwa kwa njia isiyo ya haki. Shule zao hazina rasilimali na usaidizi wa kifedha wa kutosha kama shule za weupe, na hawawezi kupata elimu bora. Aidha, ubaguzi wa rangi pia uko katika vyuo vikuu. Kwa kulingana na takwimu, wanafunzi hodari wenye asili ya Kiafrika mara kwa mara wanakabiliwa na vizuizi mbalimbali wanapotoa ombi la kusoma katika vyuo vikuu vizuri. Licha ya hayo, Wamarekani wengi wenye asili ya Kiafrika hawana uwezo wa kulipa ada ya masomo kwa watoto wao kutokana na umaskni. Ni vigumu kwa vijana weusi wa kizazi kipya ambao hawapati elimu nzuri kupata kazi nzuri, na wataendelea kuwa watu maskini.