Mawasiliano ya kitamaduni yahimiza maelewano kati ya watu wa China na Afrika
2024-04-18 14:45:45| Cri

Mwandishi mwenye asili ya Tanzania aliyeshinda Tuzo ya Nobel ya Fasihi mwaka 2021 Abdulrazak Gurnah, hivi karibuni alitembelea China na kuzungumza na mwandishi wa China Mo Yan, ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi.

Katika miaka ya hivi karibuni, mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Afrika yameongezeka, na yamefanya kazi muhimu katika kuzidisha maelewano kati ya watu wa pande hizo mbili.

Gurnah alizaliwa Zanzibar, Tanzania, na kazi zake za kifasihi haswa ni kuhusu maisha ya watu wa Afrika Mashariki. Mo Yan ni mwandishi aliyezaliwa na anayeishi nchini China, na kazi zake za kifasihi ni kuhusu maisha ya Wachina. Katika mazungumzo hayo, Gurnah alisema Zanzibar ni kisiwa cha mbali barani Afrika, lakini kinaungana na kila pembe ya dunia. Zaidi ya miaka 600 iliyopita, Mchina Zheng He akiongoza msafara mkubwa wa meli alifika kisiwani hapo, na kuanzisha mawasiliano ya kitamaduni kati ya China na Waafrika. Kwa upande wa Mo, mwaka jana alitembelea Afrika Mashariki. Licha ya mandhari ya ajabu ya asili, pia aliona utamaduni mkubwa wa Kiafrika, na uhusiano wa karibu kati ya China na Afrika.

Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kukua kwa uhusiano wa kirafiki, mawasiliano ya kitamaduni kati ya China na Afrika yameongezeka, na yamekuwa daraja la kuunganisha watu wa pande hizo mbili.

Kwanza, kama msingi wa mawasiliano ya kitamaduni, mawasiliano ya lugha kati ya China na Afrika yamepata maendeleo makubwa. Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Afrika zimechukua hatua mbalimbali ili kukuza mafunzo ya lugha ya Kichina. Hatua hizo ni pamoja na kuanzisha darasa la kichina katika shule za msingi na sekondari, kufanya ushirikiano na Taasisi ya Confucius ya China, na kuanzisha mtihani wa Kichina (HSK). Wakati huohuo, China pia imeendelea kukuza mafunzo ya lugha za Kiafrika. Kwa mfano, licha ya Kiswahili na Kihausa, Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing kimezindua kozi mpya za Kizulu, Kiamhari, Kimalagasi, Kisomali na Kitswana, ili kukidhi mahitaji ya mawasiliano ya diplomasia, biashara na utamaduni kati ya China na Afrika.

Pili, mawasiliano ya kazi za fasihi, filamu na televisheni kati ya China na Afrika yameongezeka. Kwa mfano, mapema mwa mwaka 2021, vitabu vitano vya Gurnah vilivyotafsiriwa kwa Kichina vilizinduliwa nchini China, na kupokelewa vizuri na wasomaji wa China. Kwa upande wa Mo, vitabu vyake pia vinapatikana barani Afrika. Aidha, mawasiliano kati ya China na Afrika katika kazi za filamu na tamthilia yamezidi kuwa ya kina. Kwa mfano, tamthilia ya China ya Doudou na Mama Wakwe Zake ilitafsiriwa kwa Kiswahili na Kihausa na kuonyeshwa kupitia luninga kwa watazamaji wa Afrika, pia Kampuni ya Startimes ya China imeanzisha kituo cha kutengeneza filamu na tamthilia barani Afrika.

Licha ya hayo, aina nyingine za mawasiliano ya kitamaduni ikiwemo maonesho ya sanaa na muziki pia zinastawi kati ya China na Afrika. Mawasiliano hayo ya kitamaduni yamezidisha maelewano na urafiki kati ya watu wa China na Afrika, na pia yatanufaisha maendeleo ya uhusiano na ushirikiano kati ya pande hizo mbili.