Makelele ya vyombo vya habari vya Mgharibi hayazuii China kuendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa dunia
2024-04-18 14:33:49| Cri

Takwimu zilizotolewa na Idara Kuu ya Takwimu ya China zinaonesha kuwa pato la taifa la China la mwaka 2023 liliongezeka kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na mwaka 2022. Lakini likihesabiwa kwa dola za kimarekani, lilikuwa sawa ama hata chini kidogo kuliko mwaka 2022. Wakati huo huo, pato la taifa la Marekani la mwaka jana lilikua kwa asilimia 2.5, na kuchukua nafasi nyingi zaidi katika uchumi wa dunia. Baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vikaanza kushusha matarajio ya uchumi wa China, na kusema mwelekeo wa maendeleo ya uchumi wa China umebadilika, na uchumi wa China utadidimika.

Lakini wale wanaopiga makelele wamepuuza kwa makusudi ukweli kwamba ongezeko la nafasi ya Marekani katika uchumi wa dunia limetokana zaidi na mambo ya muda mfupi kama vile kupanda kwa mfumuko wa bei na kiwango cha ubadilishaji cha dola za Kimarekani. Marekani imekumbwa na mfumuko mkubwa wa bei katika miaka kadhaa iliyopita. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, benki kuu ya Marekani iliongeza riba kwa kiasi kikubwa, hali ambayo imesababisha ongezeko la kiwango cha ubadilishaji wa dola za Kimarekani. Kutokana na hali hizo, nafasi ya Marekani katika uchumi wa dunia imeongezeka. Kwa mfano, mwaka 2022, ukuaji wa pato la taifa la Marekani ulikuwa asilimia 3.8, lakini pamoja na mfumuko wa bei, ukuaji huo ulifikia asilimia 9.2. Hali hii imesababisha ongezeko la nafasi ya Marekani katika uchumi wa dunia.

Kwa upande wa China, kutokana na mfumuko wa chini wa bei na kushuka kwa kiwango cha ubadilishaji cha Renminbi, kuanzia mwaka 2022 hadi 2023 nafasi ya China katika uchumi wa dunia ilipungua kidogo. Mwaka 2023, pato la taifa la China lilikua kwa asilimia 5.2, huku pato la taifa la Marekani likikua kwa asilimia 2.5 tu. Hata hivyo, kwa sababu mfumuko wa bei wa China ni wa chini sana kuliko ule wa Marekani, na kiwango cha ubadilishaji cha Renminbi kilishuka kwa kiasi kikubwa dhidi ya dola ya Marekani, nafasi ya China katika uchumi wa dunia ilishuka ikilinganishwa na Marekani.

Hata hivyo, ustawi wa muda wa uchumi wa Marekani hauwezi kubadilisha mwelekeo wa nguvu ya uchumi duniani. Tangu miaka ya 1970, nafasi ya Marekani katika uchumi wa dunia imekuwa ikishuka polepole, japo baadhi ya wakati iliongezeka kwa muda kutokana na athari ya mfumuko wa bei na kiwango cha ubadilishaji wa fedha. Wachambuzi wanaona kuwa nafasi ya Marekani katika uchumi wa dunia itapungua katika miaka michache ijayo. Mashirika ya kimataifa likiwemo Shirika la Fedha Duniani (IMF) yanakadiria kwamba, mwaka 2024 ukuaji wa uchumi wa Marekani utapungua hadi takriban asilimia 2.

Wakati huo huo, uchumi wa China utadumisha ukuaji wa haraka. Mashirika ya kimataifa yanakadiria kuwa, mwaka huu, ukuaji wa uchumi utafikia karibu asilimia 5, pamoja na kiwango cha mfumuko wa bei, ukuaji huo utafikia asilimia 6, ambao ni juu zaidi kuliko Marekani. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na IMF kuhusu uchumi wa dunia, kuanzia mwaka 2024 hadi 2028, nafasi ya Marekani katika uchumi wa dunia itakuwa na mwelekeo wa kushuka, huku nafasi hiyo ya China ikiendelea kupanda.