Ushirikiano kati ya China na Afrika katika magari ya nishati mpya una mustakabali mzuri
2024-04-18 14:38:27| Cri

Adam Selassie ni dereva wa basi dogo mjini Addis Ababa, Ethiopia. Siku hizi anafurahi sana, kwani amepata gari jipya la umeme. Gari hilo limeagizwa kutoka China, na hadi sasa, kuna madereva wengi kama Adam ambao wamebadilisha msbasi yao yanayotumia petroli kuwa mabasi ya umeme. Kwa maoni yao, magari ya umeme ni mazuri zaidi, kwani hayaleti makelele na uchafuzi, pia bei ya umeme ni nafuu kuliko petroli.

Ethiopia haina rasilimali za mafuta na gesi asilia, hali ambayo inailazimisha kuagiza mafuta ya bei ghali kutoka nchi za nje. Wakati huohuo, katika miaka kadhaa iliyopita, nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika upatikanaji wa umeme wa bei nafuu unaozalishwa kwa nishati safi kama vile maji, jua, upepo na joto la ardhini. Mwezi Februari mwaka huu, Wizara ya Uchukuzi na Usafirishaji ya Ethiopia ilitangaza kuwa nchi hiyo itapiga marufuku uingizwaji wa magari ya petroli na dizeli, na badala yake itaendeleza matumizi ya magari ya nishati mpya ili kukabiliana na uchafuzi wa hewa na uhaba wa mafuta.

Wakati huo huo, China inaongoza katika teknolojia na uwezo wa kuzalisha magari ya umeme, na imeshika nafasi ya kwanza duniani kwa miaka tisa mfululizo katika uzalishaji na mauzo ya magari ya umeme. Mwaka jana, ilizalisha magari karibu milioni 10 ya umeme, na kati ya hayo, zaidi ya milioni 1.2 yaliuzwa kwa nchi za nje.

Mara baada ya Ethiopia kutoa sera mpya kuhusu magari, kampuni za nchi hiyo zilianza kushirikiana na kampuni za magari ya nishati mpya za China. Basi dogo la umeme lililotajwa hapo awali limeundwa na kampuni ya Belayneh Kindie Metal Engineering Complex ya Ethiopia kwa kuagiza vipuri kutoka China. Aidha, kampuni hiyo pia imeanza kuagiza vipuri vya mabasi makubwa ya umeme kutoka China, na mabasi makubwa ya umeme yenye WIFI yanatarajiwa kutumika mjini Addis Ababa ndani ya miezi mitatu ijayo. Kama hatua inayofuata, serikali ya Ethiopia inapanga kutumia bustani zake za viwanda zilizojengwa kwa msaada wa China kuvutia kampuni za magari ya nishati mpya za China kuwekeza na kuzalisha magari ya umeme nchini humo.

Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na ongezeko la wasiwasi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na usalama wa nishati, Afrika inatilia maanani sana maendeleo ya magari ya nishati mpya. Kama nchi inayoongoza duniani katika teknolojia na uwezo wa kuzalisha magari ya nishati mpya, China inaweza kuwa mwenzi mzuri wa Afrika katika sekta ya magari ya nishati mpya.

Kwanza, Afrika ina soko kubwa la magari ya nishati mpya. Kama bara lenye idadi kubwa ya watu, Afrika inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa nishati na uchafuzi wa mazingira. Aidha, kutokana na maendeleo ya uchumi, mahitaji ya magari ya kisasa yanazidi kuongezeka barani humo. Ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika katika sekta ya magari ya nishati mpya unaweza kukidhi mahitaji hayo na kuzisaidia nchi za Afrika kujenga mfumo endelevu wa usafiri.

Pili, ushirikiano kati ya China na Afrika katika magari ya nishati mpya utatoa msaada wa kiufundi na uzoefu kwa Afrika. China imepata mafanikio makubwa katika teknolojia ya magari ya nishati mpya na ina uzoefu mkubwa. Kupitia ushirikiano na China, nchi za Afrika zinaweza kuimarisha uwezo wao na kuchochea maendeleo ya sekta ya magari ya nishati mpya.

Mbali na hayo, ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta ya magari ya nishati mpya utainua kiwango cha ushirikiano wa pande hizo mbili. Ikiwa nchi inayoongoza duniani katika sekta ya magari ya nishati mpya, ushirikiano wake na nchi za Afrika utaisaidia kupata soko kubwa na kujiendeleza zaidi. Wakati huo huo, nchi za Afrika pia zinaweza kufaidika na teknolojia na uzoefu wa China, ili kuharakisha mchakato wa maendeleo ya viwanda.