Umoja wa Afrika umetoa mwito wa kuhimiza nchi za Afrika kujenga uwezo katika sekta ya mtandao wakati nchi hizo zikikabiliwa na matishio ya mtandaoni yanayoongezeka siku hadi siku.
Mwito huo ulitolewa katika kongamano lenye kaulimbiu ya diplomasia ya mtandao linalohudhuriwa na wajumbe wa tume za kidiplomasia za nchi wanachama wa Umoja huo Aprili 15 na 16 katika makao makuu ya Umoja wa Afrika huko Addis Ababa.
Mkuu wa kitengo cha diplomasia, uchaguzi na katiba katika kamati ya Umoja wa Afrika, Bw. Calixte Aristide Mbari, amesema nchi za Afrika zinahitaji kufanya juhudi za pamoja kutatua changamoto mtandaoni.
Kwa mujibu wa Umoja wa Afrika, malengo makuu ya kongamano hilo ni kuanzisha njia ya kuingia kwa juhudi za diplomasia za mtandaoni katika Umoja wa Afrika, kuinua utambuzi wa matishio ya mtandaoni na vipaumbele vya usalama wa mtandaoni, na kufanya mazungumzo kati ya jumuiya ya kidiplomasia kuhusu asili na kiwango cha tishio.