Afrika haihitaji kufundishwa jinsi ya kuchagua marafiki zake
2024-04-18 14:46:54| Cri

“Tunawaambia moja kwa moja kwamba hamwezi kutulazimisha kuchagua marafiki zetu. Tunafikiri China ni rafiki yetu mkubwa, na hakuna mtu anayeweza kutufanya tuachane. Ni ujinga kuona kuwa sisi Waafrika hatuwezi kufikiria.”

Maneno haya yamesemwa na balozi wa Rwanda nchini China James Kimonyo. Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya nchi za Magharibi haswa Marekani zimekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la ushawishi wa China barani Afrika. Mara kwa mara zinatoa madai ya uwongo ikiwemo China inatekeleza “ukoloni mamboleo” barani Afrika, au China inaweka “mitego ya madeni” kwa nchi za Afrika, ili kudhoofisha uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika. Hata zinajaribu kuzilazimisha nchi za Afrika kuchagua upande mmoja kati ya China na Marekani. Vitendo hivyo viovu vimepingwa kabisa na nchi za Afrika.

Balozi Kimonyo ametoa kauli hiyo katika hafla iliyofanywa hivi karibuni na Ubalozi wa Rwanda nchini China ili kuadhimisha miaka 30 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994. Amesema, mauaji ya kimbari yaliharibu kabisa jamii na uchumi wa Rwanda, lakini Rais Paul Kagame wa Rwanda ameijenga upya nchi hiyo kupitia mageuzi mapana, ambapo uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa haswa China umechukua nafasi kubwa sana. Amesema China imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono ajenda ya ukaratabi wa jamii na uchumi nchini Rwanda, na uwekezaji wake katika sekta mbalimbali umetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Rwanda.

Mwaka 2018, China na Rwanda zilisaini makubaliano ya kujenga kwa pamoja “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Hadi sasa, barabara zilizojengwa na makampuni ya China zinachukua zaidi ya asilimia 70 ya barabara nchini Rwanda. Miradi ya ushirikiano ikiwemo jengo la serikali, Shule ya Ufundi ya Musanze, na visima 200 vya maji vimekamilika na kuanza kutumika, na miradi mingine ikiwemo upanuzi wa Hospitali ya Masaka, Elimu ya Akili Bandia na awamu ya pili ya Kituo cha Umeme wa Maji cha Mto Nabaronga inaendelea kutekelezwa kwa kasi. China pia ni mwenzi mkubwa zaidi wa kibiashara wa Rwanda, na thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili inakaribia dola milioni 480 za kimarekani mwaka 2022. Kuanzia Septemba mwaka 2022, China imesamehe ushuru wa asilimia 98 ya bidhaa zinazotoka Rwanda.

Alipozungumzia kauli ya nchi za Magharibi kwamba China inaweka “mtego wa madeni” barani Afrika kupitia pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, Kimonyo amesema shutuma hiyo haina mantiki. Amesema viongozi wa Afrika wanapokutana na viongozi wa China, wanajadili miradi hiyo kulingana na maslahi ya taifa husika.

Kimonyo anaamini kuwa China ni rafiki wa kweli wa Afrika, na kusema wakati China bado ilikuwa maskini sana, hayati kiongozi wake Mwenyekiti Mao Zedong alianza kusaidia Afrika. Katika miaka ya 1960, China iliunga mkono Afrika kujenga miundombinu mingi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya TAZARA inayounganisha Tanzania na Zambia.