Burundi imeomba msaada wa kimataifa kwa ajili ya wahanga wa mafuriko yaliyosababishwa na athari za El-Nino.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Umma wa Burundi Martin Niteretse amesema kwa karibu karne mbili, Burundi imekuwa miongoni mwa nchi 20 zilizo hatarini zaidi duniani kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Athari za El-Nino zimesababisha kuongezeka kwa kina cha maji ya Ziwa Tanganyika, hali iliyoleta maporomoko ya udongo, mvua kubwa na upepo mkali.
Kwa mujibu wa ofisa huyu, kati ya Septemba mwaka 2023 hadi Aprili 7 mwaka huu, zaidi ya watu laki mbili waliathiriwa na athari za El Nino, wakiwemo elfu 20 waliopoteza makazi. Mbali na hayo, hekta elfu 40 za mashamba zimesombwa na maji.
Mpaka sasa, serikali ya Burundi na washirika wa kimataifa wametoa misaada ya mbegu, pesa, chakula, huduma za afya na usafi binafsi na maji safi ya kunywa kwa wahanga wa mafuriko.