Ndege kubwa ya abiria ya C919 ya China hivi karibuni iliwasili nchini Singapore ili kushiriki kwenye Maonyesho ya Ndege ya Singapore ya mwaka 2024 yanayofanyika siku hizi. Hii ni mara ya kwanza kwa ndege kubwa aina ya C919 ya COMAC inayozalishwa nchini kuonekana nje ya nchi. Hali hii inaonesha kuwa ndege hiyo iliyotengenezwa na China imeanza kuingia katika soko la kimataifa.
Utengenezaji wa ndege kubwa unajulikana kama kilele cha kiwango cha viwanda. Kwa muda mrefu, soko la ndege kubwa za abiria duniani lilihodhiwa na Kampuni ya Boeing ya Marekani na Kampuni ya Airbus ya Ulaya. Kampuni ya Bombardier ya Canada na Kampuni ya Mitsubishi Heavy Industries ya Japan ziliwahi kujaribu kutengeneza ndege kubwa za abiria, lakini zote zilishindwa baada ya juhudi za miaka mingi.
C919 imekaribishwa na soko la safari za anga tangu ilipokamilika na kuanza kujaribiwa. Kutokana na idara husika ya China, uwezo wa uzalishaji wa C919 kwa mwaka utafikia 150 katika miaka mitano ijayo, na hadi sasa, ndege hiyo imepata zaidi ya oda 1,200 za ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na 20 zilizoagizwa na Kampuni ya General Motors ya Marekani. Katika siku zijazo, C919 inatarajiwa kuwa ndege ya tatu ya abiria kwa ukubwa duniani baada ya Boeing na Airbus.
Mafanikio ya ndege ya C919 yameonesha hatua kubwa iliyopigwa na China katika sekta ya utengenezaji. Tukichunguza mchakato wa utafiti na utengenezaji wa C919, tunaweza kugundua kwamba ndege hiyo imehusisha karibu teknolojia zote za juu.
Ndege moja ya C919 ina vipuri zaidi ya milioni 2.5, na kila sehemu ni muhimu kwa usalama na ufanisi wa safari ya ndege, hali ambayo inaonyesha kikamilifu kwamba, sekta ya utengenezaji ya China imefikia kiwango cha juu sana.
Baada ya mafanikio ya safari ya kwanza ya kibiashara ya C919, baadhi ya watu wamesema sehemu nyingi za ndege hiyo, ikiwa ni pamoja na injini, zimeagizwa kutoka nchi nyingine, wakijaribu kufumbia macho ukweli kuwa ndege hiyo imebuniwa na kutengenezwa na China. Lakini wanasahau kwamba, hivi leo, uvumbuzi wa kujitegemea unaendana na ushirikiano wa kimataifa. Ikilinganishwa na Boeing na Airbus, C919 imechelewa sana, hivyo ni afadhali itumie baadhi ya teknolojia ambazo tayari zipo. Zaidi ya hayo, ikilinganishwa na ndege kubwa nyingine, utengenezaji wa C919 umetegemea zaidi kampuni za ndani. Kwa mujibu wa orodha ya watoaji vipuri, asilimia 90 ya vipuri vya C919 vimetoka kwenye kampuni za China, na hiki ni kiwango cha juu zaidi ikilinganishwa na kampuni za nchi nyingine za kutengeneza ndege kubwa. Aidha, kuhusu suala la injini, injini ya China aina ya “Yangtze River 1000A” inayofaa kwa ndege kubwa, imefanyiwa majaribio kwa mafanikio, na inatarajiwa kuchukua nafasi ya injini zinazotoka nje ya nchi mapema iwezekanavyo.
Katika miaka ya hivi karibuni, kutoka reli ya mwendo kasi hadi ndege kubwa ya abiria, na kutoka kituo cha anga ya juu hadi manowari ya kubeba ndege za kivita, China imepiga hatua kubwa katika sekta yake ya utengenezaji. Ikiwa nchi ya kwanza kwa utengenezaji duniani, China bila shaka itatoa mchango mkubwa zaidi katika kutuliza na kuboresha mnyororo wa ugavi duniani.