Kenya yajitolea kuimarisha ushirikiano wa maendeleo na mashirika ya Umoja wa Mataifa
2024-04-18 08:41:33| CRI

Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua ameyahakikishia mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Kenya ushirikiano kutoka kwa serikali katika utekelezaji wa malengo yao ya maendeleo.

Bwana Gachagua amesema mfumo wa ushirikiano wa Umoja wa Mataifa kwa Kenya unaunga mkono na kuendana na vipaumbele vikuu vya maendeleo vya serikali, kiuchumi na kijamii.

Akiongea mjini Nairobi kwenye mkutano na mashirika 24 ya Umoja wa Mataifa nchini Kenya, Bw. Gahagua ameupongeza Umoja wa Mataifa Kenya kwa kuweka mikakati ya programu za pamoja zinazoendelezwa na wizara husika na mashirika ya Umoja wa Mataifa, pamoja na wadau mbalimbali. Ametaja programu za pamoja zinazoungwa mkono na Umoja wa Mataifa zinashughulikia vipaumbele vinavyoendana na Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kutoka mashinani (BETA) na Mpango wa Nne wa Muda wa Kati uliozinduliwa hivi karibuni (MTP IV).