Ofisi ya Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema waasi wenye silaha wameshambulia kijiji cha Kologbota katika jimbo la Mbomou nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na kusababisha mauaji ya raia 14 na kuwajeruhi wengine kadhaa huku nyumba nyingi zikichomwa moto. Taarifa inasema kundi la waasi la UPC limefanya shambulizi hilo Jumapili iliyopita kutokana na kuwashuku wanakijiji wa kijiji hicho wanashirikiana na jeshi la CAR.
Kwa mujibu wa OCHA, mashambulizi yaliyofanywa na makundi yenye silaha yameongezeka hivi karibuni nchini humo. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema Ujumbe wa walinda amani wa UM nchini CAR (MINUSCA) umeweka doria kwenye maeneo hayo yaliyoshambuliwa, huku akitaka makundi mbalimbali yenye silaha nchini humo kusitisha mara moja vitendo vya vurugu.