Utafiti waeleza hatari wajawazito kula udongo
2024-04-18 23:34:17| cri

Watafiti kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) wamesema udongo unaoliwa na wajawazito una madhara kiafya kwa kuwa umejaa fangasi na bakteria wenye magonjwa, hivyo kuhatarisha afya zao. Pia, wamesema hata mazingira ya uandaaji wa udongo huo kutoka kwenye machimbo mpaka kwa mlaji hayako salama jambo ambalo pia ni hatari.

Madhara ya udongo kwa wajawazito yameelezwa katika moja ya utafiti miongoni mwa tafiti zaidi ya 60 zinazowasilishwa kwenye maonyesho ya Wiki ya Tafiti MUCE.

Wameishauri Wizara ya Afya kuona namna ya kutoa elimu ili badala ya kula udongo, wanawake wajawazito wale chakula kingine chenye madini yanayopatikana ndani ya udongo. Baadhi ya wajawazito ambao hupenda udongo wamesema kinachowasukuma kula ni hamu ambayo hushindwa kuidhibiti.