Mwanamke ajifungua mahakamani muda mfupi baada ya kuachiliwa huru katika kesi ya mauaji ya mtoto
2024-04-19 14:16:10| cri

Mwanamke wa Machakos alijifungua mtoto wa kike katika Mahakama ya Kithimani muda mfupi baada ya hakimu kumwachilia kwa kosa la kumuua mwanawe.

Virginia Mbinya, alikuwa akitarajia kifungo cha muda mrefu jela baada ya kukamatwa akihusishwa na kifo cha mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miezi 19. Ilikuwa wakati mchungu kwa mwanamke huyo baada ya uchunguzi wa maiti kuhusisha kifo cha mtoto huyo na njaa.

Hakimu Mkuu wa Kithimani Paul Matanda alifutilia mbali kwamba kuna mchezo mchafu uliofanyika katika kifo cha Travis Muuo alipomwachilia Bi Mbinya mnamo Aprili 15. Muda mfupi baada ya Bi Mbinya kutoka mahakamni akiwa huru, lilizuka zogo nje ya mahakama wakati aliposhikwa na uchungu.

Shughuli za mahakama hiyo zilisimama huku maafisa wa mahakama na polisi wakijaribu bila mafanikio kumkimbiza hospitalini. Alijifungua mtoto wa kike nje ya mahakama baada ya wanawake kumuwekea pazia khanga ili kujifungua.

Baada ya kujifungua, polisi na maafisa wa mahakama walimkimbiza mama huyo na mtoto wake katika Zahanati ya Kithimani.