Mjumbe wa China asema matakwa ya wapalestina ya kuanzisha nchi huru hayawezi kuepukwa
2024-04-19 09:10:18| CRI

Mjumbe wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Fu Cong amesema duru hii ya mgogoro kati ya Palestina na Israel, imeionya jumuiya ya kimataifa kwamba haiwezi tena kuepuka matakwa ya muda mrefu ya wapalestina ya kuanzisha nchi huru, na haiwezi tena kuendeleza dhulma ya kihistoria dhidi ya watu wa Palestina.

Balozi Fu Cong amesema kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama kuhusu suala la Palestina na Israel kwamba mpango wa nchi mbili lazima urudishwe.

Mgogoro kati ya Israel na Palestina umedumu kwa zaidi ya miaka 70 na Israel imepata uhuru na kujenga nchi yao, lakini haki za wapalestina kujitawala na kuanzisha nchi huru zimepuuzwa kwa muda mrefu. Kuwa nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa ni hatua muhimu kwa Palestina kuanzisha nchi huru. Palestina imeanza tena kuomba kuwa mwanachama rasmi wa Umoja wa Mataifa, China inatoa wito kwa wanachama wote wa baraza la usalama kupiga kura ya ndio kuunga mkono ombi hilo la Palestina.