Kwa nini wasema soko la China linavutia zaidi?
2024-04-19 14:26:36| cri

Maonyesho ya 4 ya Kimataifa ya Bidhaa za Matumizi ya China (CICPE) ya mwaka huu yaliyofanyika mkoani Hainan, yameshirikisha chapa zaidi ya 4,000 kutoka nchi na sehemu 71 duniani, na idadi ya makampuni na ile ya chapa kutoka nje ya nchi zimeweka rekodi mpya. Katika maonesho hayo, bidhaa mpya 1,462 zilizinduliwa, na chapa 84 za ndani na za nje ya nchi zilioneshwa kwa mara ya kwanza, na Uingereza, Mongolia na Malaysia zilishiriki kwa mara ya kwanza.

Soko ni rasilimali inayokosekana zaidi. Kwa makampuni ya kigeni, soko kubwa la China linamaanisha mapato makubwa. Hivi sasa China inajitahidi kupanua matumizi baada ya kufufuka kwenye janga la COVID-19. Katika robo ya kwanza ya mwaka huu, matumizi yamechangia asilimia 73.7 ya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP). Mwezi Aprili, viashiria vya ustawi wa biashara ya rejareja ya China (CRPI) ilifikia asilimia 50.4, ikiwa katika kiwango cha ukuaji kwa mwaka mzima. Uhai wa matumizi vilevile umeoneshwa moja kwa moja katika uendeshaji biashara wa makampuni ya kigeni. Wakuu wengi wa makampuni wamesema kuwa soko la China linajaa fursa na pia lina uwezo mkubwa wa ushindani, na kwamba wanaamini kuwa soko la China litaendelea kukua.

Mbali na hayo, mazingira ya kufanyia biashara nchini China yaliyo wazi na yenye sifa bora yameyafungulia makampuni ya kigeni dirisha la mustakabali. Haswa baada ya kutekelezwa kwa sera ya “kuongeza nchi 59 zinazosamehewa viza kuingia mkoa wa Hainan” mwezi Februari mwaka huu, wageni wengi waliweza kushiriki maonesho hayo bila ya viza. Hatua hii inaonyesha kwamba China inafungua mlango kwa kiwango cha juu zaidi. Kutoka kurahisishwa kwa hatua mfululizo za kuingia na kutoka kwenye forodha ya China na ulipaji wa fedha, hadi kutekelezwa kwa sera zenye nguvu kubwa zaidi za kuvutia na kutumia fedha za kigeni, na kulingana na kanuni za kimataifa za kiuchumi na kibiashara, mlango wa China umefunguliwa na kuwa wazi zaidi, na nafasi za maendeleo kwa makampuni ya kigeni nchini China zitakuwa kubwa zaidi.