EIB na Mfuko wa Gates washirikiana kuwawezesha wanawake wa Kenya
2024-04-19 23:14:39| cri

Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Mfuko wa Bill and Melinda Gates Alhamisi walizindua ushirikiano mpya ili kuimarisha nguvu ya kiuchumi ya wanawake nchini Kenya katika kukabiliana na vikwazo muhimu vya ushirikishwaji kifedha.

Ushirikiano huo unaongoza mpango mpya wa utoaji mikopo ya dola za Kimarekani milioni 31.95 nchini Kenya, unaofadhiliwa na Benki ya EIB Global na Benki ya KCB Kenya kwa dola milioni 15.97.

Katika taarifa iliyotolewa mjini Nairobi, Kenya balozi wa EU nchini Kenya Henriette Geiger, alisema Kenya na Umoja wa Ulaya zimeazimia kuleta usawa wa kijinsia na kwamba ushirikiano huo mpya utaongeza fursa na kuboresha maisha ya maelfu ya wanawake na familia zao nchini Kenya na kote barani Afrika.

Mpango huo umeanzishwa ili kuhakikisha asilimia 80 ya wanufaika watakuwa wanawake, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa fedha kwa wakopaji ambao hawana mali za kuweka dhamana au historia ya mikopo, bei iliyorekebishwa ili kushughulikia viwango vya juu vya riba, kutumia huduma za kidigitali kwa mahitaji maalum ya wakopaji wa kike na kuboresha ujuzi wa kifedha.