Rais wa Kenya atoa wito wa kuoanishwa kwa sera za TEHAMA kote barani Afrika
2024-04-23 09:27:41| CRI

Rais wa Kenya William Ruto Jumatatu alitoa wito wa kuoanishwa kwa sera za teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kote barani Afrika ili kuchochea mageuzi ya kidijitali.

Rais Ruto aliyasema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa “Afrika iliyounganishwa wa 2024”, ulioanza mjini Nairobi, nchini Kenya. Amefafanua kuwa ushirikiano huo unapaswa kuongozwa na mtandao wa mamlaka za TEHAMA na kusimamiwa na ujumuishaji wa mipango ya mabadiliko ya kidijitali. Ruto alisema kuwa kuoanisha sera za kidijitali katika bara zima kutasaidia kuharakisha azma ya Afrika kujiweka mbele kabisa kwenye biashara ya kimataifa, hasa kwenye utekelezaji wa makubaliano ya Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA).

Katika habari nyingine Kampuni ya Usambazaji Umeme ya Kenya, imesema itawekeza dola milioni 1.93 za Kimarekani katika miaka mitatu ijayo ili kuchochea matumizi ya magari ya umeme nchini humo. Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Joseph Siror alisema uwekezaji huo unajumuisha gharama ya ununuzi wa magari na pikipiki za umeme ili kusaidia shughuli za biashara pamoja na uanzishaji wa vituo vya kuchaji katika maeneo mbalimbali kote nchini.