Kampuni ya teknolojia ya China, Huawei ilisema Jumatatu kwamba inaongeza kasi ya kusambaza miundombinu ya mtandao wa mawasiliano kwa kaya zenye kipato cha chini nchini Kenya ili kukuza uchumi wa kidijitali nchini humo.
Akiongea kando ya Mkutano wa ‘Afrika iliyounganishwa wa 2024’, uliofanyika mjini Nairobi chini ya kaulimbiu "Kuunda Mustakabali wa Afrika Iliyounganishwa: Kufungua Ukuaji Zaidi ya Muunganisho", Mkurugenzi wa masuala ya serikali na ushirikiano wa Huawei nchini Kenya, Adam Lane, alisema kwamba nyumba nyingi za kiwango cha juu zina chaguo la kuunganishwa na mtandao wa mawasiliano, ukiwemo mkonga wa mawasiliano, tofauti na makazi ya watu wa kipato cha chini.
Amebainisha kuwa wana teknolojia mahususi kwa ajili ya kaya zenye kipato cha chini ambazo zinarahisisha kuunganishwa kwa mtandao wa mawasiliano na kutumia vifaa vichache, jambo ambalo husaidia kupunguza gharama na kuongeza kasi ya upatikanaji wa intaneti.
Hafla hiyo ya siku tano iliwaleta pamoja mawaziri na wadhibiti wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kutoka nchi 35 za Afrika, pamoja na maafisa wa Umoja wa Ulaya, ili kutafuta njia za kupunguza mgawanyiko wa kidijitali barani Afrika.