Kenya yazitaka nchi za Afrika kukumbatia Akili Bandia kwenye ushirikishwaji wa kijamii
2024-04-24 09:33:42| CRI

Kenya imezihimiza nchi nyingine za Afrika kukumbatia nguvu ya teknolojia ya akili bandia (AI) ili kutekeleza ajenda ya maendeleo ya bara hilo.

Akiongea kwenye Mkutano wa kuunganisha Afrika ambao ni kongamano la teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) barani kote lililofanyika Nairobi nchini Kenya, katibu mkuu wa Idara ya Taifa ya Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari na Uchumi wa Dijitali ya Kenya John Tanui amesema kuwa teknolojia ya kidijitali, haswa Akili Bandia, itakuza ushirikishwaji wa kijamii katika bara zima.

Ameongeza kuwa wana nia ya dhati kama Wakenya kutumia nguvu ya mabadiliko ya teknolojia ya AI ili kuendeleza ajenda ya maendeleo. Hii inaambatana na matarajio makubwa yaliyowekwa katika malengo ya miaka 50 ya maendeleo ya bara la Afrika, Agenda 2063. Malengo hayo yananasa dira ya Afrika ya kuwa bara lenye ustawi, jumuishi na la amani linaloendeshwa na raia wake.