UNECA yasema kuongezeka kwa mzigo wa deni la umma na kupungua kwa nafasi ya kifedha kunaiweka Afrika katika njia panda
2024-04-24 09:38:57| CRI

Katibu mtendaji wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ya Afrika (UNECA), Claver Gatete amesema kuongezeka kwa mzigo wa deni la umma kutokana na majanga yanayohusiana na hali ya hewa na kupungua kwa nafasi ya kifedha kwa sababu ya kuongezeka kwa mahitaji ya kifedha kumeiweka Afrika katika njia panda.

Hayo aliyasema Jumanne katika ufunguzi wa Kongamano la 10 la Kanda ya Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu huko Addis Ababa, Ethiopia. Kaulimbiu ya kongamano hilo ni "Kuimarisha Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu na Ajenda 2063 na kutokomeza umaskini wakati wa majanga mengi: utoaji bora wa suluhu endelevu, thabiti na za kiubunifu."

Akisisitiza dharura ya kushughulikia changamoto muhimu zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kifedha katika bara zima, Gatete alisema miundombinu ya Afrika na mahitaji ya mabadiliko ya tabianchi yanakadiriwa kugharimu kati ya dola bilioni 68 na bilioni 108 kila mwaka.