Serikali ya Tanzania kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia
2024-04-25 10:44:20| cri

Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema, katika mwaka 2024/25, serikali ya nchi hiyo itaendelea kutekeleza hatua madhubuti za kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini humo.

Dk. Biteko amesema hayo katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2024/25. Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wengine itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 – 2034 kwa kupatia ufumbuzi vikwazo vya matumizi ya nishati hiyo, ikiwemo gharama kubwa, upatikanaji hafifu na uhaba wa miundombinu yake na kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya nishati zisizo safi na salama za kupikia.

Pia, Dk. Biteko amesema serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kusambaza majiko banifu kwenye kaya zilizopo katika maeneo ya vijijini na vijiji-miji.