China yatoa ufadhili wa chakula cha shule kwa watoto 165,000 kaskazini mashariki mwa Uganda
2024-04-25 10:14:19| CRI

Kupitia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) China imetenga fedha ili kutoa chakula shuleni kwa zaidi ya watoto 165,000 kutoka shule 315 za huko Karamoja nchini Uganda.

Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano hayo Jumatano, balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong amesema mchango huo ni sehemu ya azma ya China kuboresha usalama wa chakula na lishe, kuimarisha maisha ya watu na kukuza uchumi wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa WFP, ufadhili huo utawezesha shule za huko kununua mahindi, maharagwe na mafuta ya mboga kwa ajili ya watoto hao.

Akitoa shukrani zake kwa mchango huo, Mkurugenzi wa WFP nchini Uganda Abdirahman Meygag alisema China inaunga mkono juhudi zao za kutoa chakula shuleni kwa watoto, ambapo wameshuhudia watoto waliofaidika na mpango wa chakula shuleni wakiwa maafisa wakuu wa serikali, madaktari na wajasiriamali.

Huu unakuwa ni mpango wa tatu wa msaada wa chakula wa China katika eneo la Karamoja kupitia WFP na serikali ya Uganda. Mwaka 2018, China ilitoa tani 6,000 za chakula, na kunufaisha zaidi ya watu 200,000. Mwaka 2021, msaada wa chakula wa China ulinufaisha zaidi ya watu 120,000 katika shule 300 za eneo hilo.