Msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu Joyce Msuya amesema eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni mojawapo ya maeneo hatari zaidi duniani kwa wanawake na wasichana.
Msuya Ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano, kuwa wanawake na wasichana wanakabiliwa na unyanyasaji wa viwango vya juu katika kambi zilizojaa watu karibu na Goma, wakiishi bila ya taa wala faragha, hawana vifaa vya usafi vya kutosha, na hakuna hatua za kiusalama.
Ameongeza katika taarifa yake kuhusu hali katika eneo la Maziwa Makuu kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu Martin Griffiths, kuwa kesi zilizoripotiwa za unyanyasaji wa kijinsia nchini DRC zimeongezeka kutoka 40,000 mwaka 2021 hadi 78,000 mwaka 2022. Mwaka 2023, idadi hii ilifikia 123,000, ongezeko la zaidi ya asilimia 300 ndani ya miaka mitatu, ambalo linaendelea kuongezeka. Ameongeza kuwa cha kusikitisha ni kwamba, ukosefu wa taarifa na rasilimali chache za huduma za manusura inamaanisha kuwa idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi.