Ethiopia yatarajia uwekezaji zaidi wa China katika sekta ya viwanda
2024-04-26 10:05:33| CRI

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Maeneo ya Viwanda la Ethiopia (IPDC) Aklilu Tadesse, amesema uwekezaji wa China umetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya viwanda nchini Ethiopia, ambapo wadau wa sekta hiyo wana nia ya kuwasaidia wawekezaji wa China wanaotaka kuingia katika nchi hiyo.

Tadesse aliyasema hayo Jumatano wakati wa majadiliano na wawekezaji wa China ambao wameonesha nia yao ya kuwekeza katika maeneo ya viwanda nchini humo, na kuongeza kuwa wawekezaji wa China kwa sasa wanawakilisha kundi kubwa zaidi la wawekezaji wa kigeni katika maeneo ya viwanda yanayosimamiwa na IPDC.

Ethiopia, nchi ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika, imeelezea dhamira yake kubwa ya kuimarisha ushirikiano na China katika kuendeleza maeneo ya viwanda ili kutimiza lengo lake la kuwa kitovu cha utengenezaji wa bidhaa barani Afrika.

Katika taarifa yake, IPDC ilisisitiza azma ya Ethiopia kubakia kuwa nchi inayopendelewa zaidi na China barani Afrika kwa ajili ya kuendeleza maeneo ya viwanda na uwekezaji ndani yake.