Dunia inahitaji uzalishaji wa bidhaa za kijani wa China
2024-04-26 22:39:38| cri

Hivi karibuni maafisa wa serikali ya Marekani mara kwa mara wamelalamika kuwa China inazalisha bidhaa nyingi kupita kiasi za kijani, zikiwemo magari ya nishati mpya, betri na photovoltaic, na kudai “uzalishaji wa kupita kiasi” wa China unatishia uchumi wa dunia. Hiki ni kisingizio kipya baada ya “usalama wa taifa” kilichotolewa na Marekani ili kujilinda kibiashara.

Tangu wakati wa utawala wa Donald Trump, Marekani ilianza kutumia “usalama wa taifa” kama silaha katika biashara na nchi nyingine, na sasa serikali ya Joe Biden imekuza zaidi silaha hiyo. Kutoka bidhaa za kisasa za hali ya juu zikiwemo vifaa vya mtandao wa 6G, simu janja, na ndege zisizo na rubani za kiraia, hadi bidhaa za malighafi kama vile chuma na alumini, na hata kreni zinazotumika bandarini, Marekani imeweka vikwazo kwa kisingizio cha kulinda “usalama wa taifa”. Bila shaka kisingizio hicho kinailenga zaidi China, kwani hadi sasa, mamia ya makampuni ya China yameorodheshwa kwenye orodha nyeusi ya kibiashara ya Marekani kwa kisingizio hicho, mfano Huawei, kampuni ya China ya teknolojia ya juu. Simu janja ya Huawei iliwahi kushika nafasi ya kwanza katika soko la kimataifa, na kuleta changamoto kubwa kwa simu za iPhone zinazotengenezwa Marekani. Mwishowe, Marekani iliweka vikwazo vikali zaidi katika historia yake dhidi ya Huawei, ili kuiangamiza kabisa.

Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya nishati mpya ya China imepata maendeleo ya kasi kubwa, na kuwa na ushindani mkubwa katika soko la kimataifa. Hivyo Marekani imepata kisingizio kipya kwamba, “uzalishaji wa kupita kiasi” wa China umeleta changamoto kwa sekta hiyo katika nchi nyingine duniani, ambacho hakina mantiki zaidi kuliko kile cha “usalama wa taifa.” Kutokana na utandawazi, kutathmini kama kuna uzalishaji wa kupita kiasi hutegemea mahitaji ya kimataifa, na Marekani inapuuza hali halisi ya soko la kimataifa na kulinganisha tu mauzo ya bidhaa za China kwa nchi za nje. Lakini ukweli ni kwamba hivi sasa uzalishaji wa bidhaa za kijani hauwezi kukidhi mahitaji ya nchi mbalimbali duniani, kwani dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi. Aidha, kwa upande wa matumizi ya uwezo wa uzalishaji, China imetumia vizuri zaidi uwezo wake wa uzalishaji wa bidhaa za kijani kuliko nchi nyingine husika. Kwa mfano, kuhusu magari ya nishati mpya, takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2023 uzalishaji na mauzo ya magari ya nishati mpya nchini China yalikuwa milioni 9.587 na milioni 9.495 mtawalia, na kiwango cha matumizi ya uwezo wa uzalishaji ni karibu asilimia 80. Wakati huo huo, matumizi ya uwezo wa uzalishaji wa Kampuni ya Magari ya Hyundai ya Korea Kusini yalikuwa asilimia 23 tu.

Kwa upande wa nchi zinazoendelea, zikiwemo nchi za Afrika, bidhaa za kijani za China zenye ubora wa juu na bei nafuu zimeziletea fursa nzuri ya kupunguza pengo na nchi zilizoendelea, na pia kuziwezesha kukabiliana vizuri na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Wafanyabiashara wengi kutoka nchi zinazoendelea wanasema bidhaa nyingi za kijani zilizotengenezwa China ni za ubora wa juu zaidi duniani, na bei zake ni nafuu, na kama bidhaa hizo zingeuzwa na nchi za Magharibi, nchi zao zingeshindwa kumudu bei.

Marekani inapuuza ukweli na kuishutumu China kuzalisha bidhaa nyingi za kupita kiasi za kijani, ili kulinda kampuni zake husika. Lakini kumwangusha mwingine hakuwezi kukufanya kukimbia haraka zaidi, soko linahitaji ushindani wa kutosha ili bidhaa bora zaidi zipatikane.

 

.