Meli ya mizigo iliyosajiliwa Zanzibar, Tanzania na wafanyakazi wake watano bado haijapatikana katika Bahari ya Hindi
2024-04-26 09:59:32| CRI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema meli ya mizigo iliyosajiliwa Zanzibar na wafanyakazi wake watano wa Tanzania waliotoweka katika Bahari ya Hindi Aprili 19 bado haijapatikana.

Afisa mawasiliano wa TASAC Mariam Mwayela aliliambia shirika la habari la China Xinhua kwa njia ya simu kuwa msako wa meli na wafanyakazi wake bado unaendelea.

Meli hiyo ilitoweka huku mamlaka ya hali ya hewa ikitoa tahadhari juu ya upepo mkali wa zaidi ya kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa ya bahari ya mita mbili.

TASAC Jumatano ilisema katika taarifa yake kwamba meli hiyo iliyokuwa na tani 65 za mbao ikiwa na mabaharia watano wa Tanzania ilitoweka Aprili 19 baada ya kuondoka bandari ya Kilwa Kivinje saa moja asubuhi kwa saa za huko na ilitakiwa kuwasili katika bandari ya Malindi mjini Zanzibar saa mbili asubuhi siku iliyofuata.