Mpango wa mafunzo wa DigiTruck wa kampuni ya mawasiliano ya simu ya China Huawei, ulioanza mwaka 2019, umechangia pakubwa katika kuongeza mapato, fursa za ajira na ujasiriamali nchini Kenya.
Hayo yamo kwenye ripoti iliyotolewa siku ya Alhamisi na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali ya Kenya, ambapo inasema DigiTruck ni darasa linalohama na kutumia nishati ya jua likiwa na laptop, simu janja na mtandao wa inteneti, limekuwa na jukumu muhimu katika kuharakisha ufundishaji wa ujuzi wa kidijitali nchini Kenya. Ripoti hiyo iliyozinduliwa katika Mkutano wa “Afrika Iliyounganishwa wa 2024” imesema utafiti wa vijana waliopata mafunzo kwa muda wa miaka minne ulionyesha matokeo chanya yanayoonekana kwa walengwa. Mkutano huo wa siku nne uliwakutanisha mawaziri na wasimamizi wa TEHAMA kutoka nchi 35 za Afrika wakijadili mikakati ya kupunguza pengo la kidijitali barani Afrika.