Mahakama ya kijeshi nchini Uganda yawaachilia huru wakenya 32 waliofungwa kwa kupatikana na silaha kinyume cha sheria
2024-04-26 10:04:18| CRI

Mahakama ya kijeshi nchini Uganda imeamuru kuachiliwa kwa raia 32 wa Kenya ambao awali walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria.

Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Kijeshi (GCM), ambayo ilikutana Jumatano, ilitengua uamuzi wa awali wa mahakama ya chini. GCM iligundua ukiukwaji wa taratibu wakati wa kesi hiyo ya mwaka jana ambayo ilipelekea raia wa Kenya kufungwa jela.

Uamuzi wa GCM ulisema kwamba ingawa kundi la washtakiwa lilikubali hatia, saba kati yao walikuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 18. Kwa maana hiyo, hawakupaswa kuhukumiwa na mahakama ya kijeshi.

Nyaraka za mahakama zilifichua kuwa kundi hilo la Wakenya lilikamatwa likiwa na bunduki ndogo 28 na risasi 801 katika wilaya ya Moroto kaskazini mashariki mwa Uganda na baadaye kuhukumiwa mwezi Aprili mwaka jana. Wafungwa hao baadaye walikata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.