Ofisa wa Hamas asema hawatakubaliana na Israel ikiwa vita itaendelea Ukanda wa Gaza
2024-04-29 08:51:42| CRI

Ofisa wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas, Sami Abu Zuhri amesema, kundi hilo halitafikia makubaliano yoyote na Israel ambayo hayahusishi kumalizika kwa vita katika Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa yake, Ofisa huyo ameongeza kuwa, majibu ya Israel, ambayo yalilifikia kundi hilo kupitia wapatanishi, bado yanafanyiwa tathmini, na ni mapema sana kufikia uamuzi kuhusu majibu hayo.

Ujumbe wa Hamas unatarajiwa kuwasili katika mji mkuu wa Misri, Cairo, hii leo, kupeleka majibu ya kundi hilo kuhusu kusimamisha vita katika Ukanda wa Gaza na kufanya majadiliano kuhusu makubaliano ya kubadilishana mateka na wafungwa na Israel.

Jumamosi iliyopita, kundi la Hamas lilitangaza kuwa limepokea majibu rasmi ya Israel kuhusu msimamo wa kundi hilo katika kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza, ambayo yaliwasilishwa kwa wapatanishi kutoka Misri na Qatar April 13 mwaka huu.