Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mvutano na operesheni za kijeshi katika mji wa El Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, wajumbe wa Baraza hilo wameeleza wasiwasi wao mkubwa juu ya mashambulizi ya vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na wafuasi wake dhidi ya mji wa El Fasher, ambao unahifadhi maelfu ya watu waliokimbia vurugu kutoka sehemu nyingine za nchini humo.
Wajumbe hao wametoa wito kwa majeshi ya Sudan na vikosi vya RSF ambavyo vimekuwa vikipigana tangu tarehe 15 Aprili mwaka 2023, kusimamisha kutuma vikosi vya kijeshi karibu na El Fasher na kuchukua hatua za kupunguza hali ya mvutano wakati wa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ya kibinadamu ya kimataifa.
Aidha wajumbe hao pia wamerudia wito wao wa kusitisha mapigano mara moja, wakizitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kujizuia kuingilia kati mapigano hayo, bali kuunga mkono juhudi za amani ya kudumu. Pia wamezikumbusha pande zote zinazohusika na mgogoro huo na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuzingatia wajibu wao kuhusu vikwazo vya silaha.