China kuwa mchangiaji mkubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi wa dunia katika miaka mitano ijayo
2024-04-29 08:49:42| CRI

Shirika la habari la Bloomberg la Marekani hivi karibuni limetabiri kuwa China itakuwa mchangiaji mkubwa zaidi wa ukuaji wa uchumi duniani katika miaka mitano ijayo, huku kiwango cha mchango wake kikizidi kile cha nchi zote wanachama wa Kundi la Nchi 7 (G7) na karibu mara mbili ya kile cha Marekani.

Makadirio ya shirika hilo yanatokana na takwimu za utabiri wa uchumi zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zinazoonyesha kuwa, asilimia 75 ya ukuaji wa uchumi wa dunia katika miaka mitano ijayo unatarajiwa kujikita zaidi katika nchi 20, ambapo China, India, Marekani na Indonesia zitachangia zaidi ya nusu ya ukuaji wa uchumi wa dunia, na China itachangia karibu asilimia 21 ya shughuli mpya za kiuchumi duniani.

Mwakilishi Mkuu wa IMF nchini China Bw. Steven Barnett, hivi karibuni alieleza matumaini yake kuhusu uhai na ustahimilivu wa uchumi wa China, akiamini kuwa mwelekeo mzuri wa uchumi wa China ni muhimu kwa ukuaji wa utulivu wa kimataifa, na kwamba uchumi wa China bado ni kichocheo muhimu kwa uchumi wa dunia.