Benki ya Dunia imesema itatoa mikopo nafuu kwa nchi za Afrika na kushirikiana na serikali za nchi hizo kuwezesha maendeleo endelevu ya bara hilo.
Akizungumza katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wenye lengo la kuainisha vipaumbele vya bara hilo (IDA21), Mkuu wa Kundi la Benki ya Dunia, Ajay Banga amesema, Jumuiya ya Kimataifa ya Maendeleo (IDA) italipatia bara la Afrika fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya kijani na juhudi za kuondokana na umasikini.
Amesema kuna hadithi nyingi za mafanikio katika nchi zilizopata ufadhili wa IDA na kubadili uchumi wao, akitoa mfano wa China, ambayo imebadilika kutoka mkopaji wa IDA mpaka kuwa mkopeshaji wa Jumuiya hiyo na kuondoa mamilioni ya raia wake katika umasikini.
Akizungumza kwenye Mkutano huo, Rais wa Kenya William Ruto ametoa wito wa kuongeza ufadhili wa kifedha kwa ajili ya Jumuiya ya Kimataifa ya Maendeleo, akisema inapaswa kuongezwa kutoka dola bilioni 93 ya mwaka 2022 hadi dola bilioni 120 mwaka huu.