Somalia na mashirika ya Umoja wa Mataifa yatoa wito wa kuongeza kasi ya utoaji wa chanjo
2024-04-30 09:06:59| cri

Somalia na mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa pamoja walitoa wito kwa washirika na wafadhili kuongeza kasi ya utoaji wa chanjo ili kufikia kila mtoto nchini Somalia.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana, Waziri wa Afya wa Somalia Bw. Ali Haji Adam Abubakar amesema, migogoro ya muda mrefu na kukosekana kwa utulivu katika miongo michache iliyopita kumesababisha mfumo dhaifu wa afya, uliogawanyika na ambao haukufadhiliwa sana nchini Somalia.

Amesema kutambulishwa kwa chanjo mpya kama chanjo ya kuzuia homa ya mapafu na kuhara baadaye mwaka huu kutaisaidia Somalia kukabiliana na homa ya mapafu na kuhara, magonjwa ambayo yanachangia vifo vya watoto nchini Somalia.

Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Bw. Wafaa Saeed alisema, tishio la magonjwa yanayozuilika kwa chanjo bado liko juu nchini Somalia, huku takriban watoto milioni 1.5 chini ya miaka mitano wakijulikana kama watoto wa "dozi sifuri".