Watu 40 wafariki baada ya bwawa kubomoka kutokana na mvua kubwa nchini Kenya
2024-04-30 09:06:36| CRI

Polisi nchini Kenya imesema, watu 40 wamethibitishwa kufariki huku wengine wengi hawajulikani walipo baada ya bwawa lililopo kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi, kubomoka kufuatia mvua kubwa zinazonyesha nchini humo.

Kamanda wa Polisi wa Naivaha, Stephen Kirui amesema, jana, Polisi wamepata miili 40 iliyozama katika tope, huku operesheni kubwa ya uokoaji ikiendelea katika eneo la Mai Mahiu baada ya mto ulio karibu kujaa maji kutokana na mafuriko ya ghafla.

Maofisa wa eneo hilo wanasema huenda idadi ya vifo inaweza kuongezeka wakati operesheni ya uokoaji ikiendelea kwa kuwa watu wengi bado hawajulikani walipo.

Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura amesema, mvua kubwa zinazonyesha zimeathiri kaunti zote 47 nchini humo, na mafuriko yamezifanya kaya 24,196 kukosa makazi.