Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya nchi za Afrika Mashariki (IGAD) zimezindua mradi wa kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na majanga katika kanda hiyo.
Mradi huo unaopokea ufadhili kutoka kampuni ya Google unalenga kuboresha mwitikio wa changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa ambazo zimeongezeka katika kanda ya Pembe ya Afrika.
Mkurugenzi wa Kituo cha Hali ya Hewa (ICPAC) kilicho chini ya IGAD, Guleid Artan amesema, mradi huo unalenga kufufua mifumo ya tahadhari za mapema katika kanda hiyo na kuongeza uwezo wa jamii katika maeneo husika kugundua na kuwa tayari kwa majanga.
Kupitia matumizi ya akili bandia, mafunzo ya kutumia mashine, na uchambuzi wa data, mradi huo unalenga kuongeza usahihi na muda wa tahadhari za majanga, kuwezesha jamii kuchukua hatua sahihi kuokoa na kulinda maisha yao.