Kuhimiza wanawake na watoto wa kike kushiriki katika mambo ya sayansi na teknolojia
2024-05-03 08:26:18| CRI

Hivi karibuni ulifanyika mkutano wa uvumbuzi wa wanawake wanaoshughulikia mambo ya sayansi na teknolojia duniani mwaka 2024. Mkutano huu uliofanyika Aprili 27, ulikuwa na kauli mbiu ya "Kuchochea Uhai na Msukumo wa Wanawake". Kihistoria, uwepo wa wanawake katika nyanja za teknolojia na sayansi umekuwa mdogo sana ukilinganisha na ule wa wenzao wanaume. Hata wakati wanawake wanapochangia katika nyanja hizi, machapisho yanayoelezea kazi zao yanakuwa machache pia. Kwa kuwa Nyanja ya historia ya sayansi na teknolojia imekuwa ikitawaliwa na wanaume, hamu ya kuandika juu ya michango ya wanawake katika nyanja hizi pia imekuwa ndogo.

Ni kweli, hata hivyo, muelekeo huu umekuwa ukibadilika polepole katika miaka ya hivi karibuni. Wanawake wengi zaidi siku hizi wanaingia katika nyanja za sayansi na uhandisi, pamoja na historia ya sayansi na teknolojia, na pia idadi inayoongezeka ya vyuo vikuu sasa vinajitahidi kuvutia wanawake zaidi katika sayansi na uhandisi. Kwa upande wa shule za msingi pia zinafanya juhudi za ziada kuwaleta wasichana katika nyanja za sayansi na uhandisi tangu wakiwa wadogo. Hivyo leo katika kipindi cha ukumbi wa wanawake tutaangazia juhudi zinazofanywa ili kuhimiza wanawake na watoto wa kike kushiriki katika mambo ya sayansi na teknolojia.